Welcome to Blogster!
810,398 Blogster Users  |  364,642 Posts
 
 
 

saiboko

 

Blog Traffic: 38710

Posts: 97

My Comments: 15

User Comments: 94

Photos: 77

Friends: 11

Following: 0

Followers: 0

Points: 1458

Last Online: 1289 days ago


 
 

Visitors

No Recent Visitors
 

Kivuko Kigamboni Kulikoni?

Added: Thursday, May 24th 2007 at 3:03am by saiboko
Related Tags: legal, politics
 
 
 

Makala hii ilichapishwa kwenye gazeti la fahamu 5/3/2007


Kivukoni

Wakiambiwa hawaamini mpaka waone. Lakini sikuzote majuto ni mjukuu kwa vile mambo mwisho huja kinyume. Lakini mwanadamu ni kiumbe mkaidi na mwenye hila nyingi ndio maana wengine wakasema “duniani kuna watu wengi sana lakini binadamu ni wachache sana”. Msemo huu ni muhimu sana na wala sio nadharia ila ni ukweli usiopingika.

Nimetumia maneno hayo hapo juu kwa vile nataka kujadili suala la msingi sana hapa kwenye makala hii. Suala lenyewe linahusiana na sekta ya usafirishaji Tanzania. Kuna mambo mengi yakujadili lakini ningependa kuelekeza macho yangu pale Feri au Kivukoni Dar es salaam.

Itakumbukwa kwamba ni miaka kadhaa sasa wananchi wa Dar es salaam wamekua wakilalamikia usafiri wa Kigamboni kwamba ni hatari sana kwa maisha yao. Wakati fulani serikali ilitangaza mikakati ya kujenga daraja la kuunganisha Kigamboni na maeneo mengine ya Dar es salaam. Lakini miaka inapita na hakuna kinachoendelea.

Inafikia hatua sasa wananchi wa Kigamboni wanajiona kama wametolewa kafara. Na hii nikutokana na ukweli kwamba Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ilishaishauri Serikali isimamishe usafiri wa MV Kigamboni kwasababu ni hatari kwa usalama wa maisha ya raia. Lakini mpaka leo Pantoni hiyo bado inafanya kazi ya kuvusha wananchi.

Lakini hali ilivyo sasa ni hatari zaidi kwasababu hata kivuko kingine cha MV Alina nacho nikibovu sana. Hufikia wakati vyote viwili vikawa havifanyi kazi. Wakati mwingine vinaharibikia katikati ya bahari na kupoteza muelekeo. Kwa mfano kunasiku kivuko kilikaa majini kwa muda wa masaa matatu, siku nyingine kilipoteza muelekeo kikaelekea Kurasini badala ya Kigamboni, wakati mwingine wananchi wanashukia majini kwavile kivuko kinashindwa kufika sehemu ya kushushia abiria.

Sitosahau siku ambayo mimi na rafiki yangu tulikua tunatoka Kigamboni tunaelekea mjini tukiwa tunasafiri ndani ya MV Kigamboni. Safari ilikua nzuri na tukafika upande wa pili salamasalimini, tatizo lilikuja wakati wa kushuka. Mwenzangu alishawasha gari anajiandaa kutoa ndani ya kivuko, mara ghafla Kivuko kikaanza kuruki nyuma kama mita tano hivi ndani ya maji. Kitendo hicho kilisababishwa na ubovu wa kivuko hicho. Hata hivyo ilichukua muda kidogo mpaka tukafanikiwa kurudi tena eneo la kushukia. Tulipokua tumeshatoka mwenzangu akaniuliza unaonaje kama tungeshatoa magurudumu ya mbele? Nikamjibu tungekua tumezama. Tukamshukuru Mungu na safari ikaendelea.

Wakati huo ndio dereva akanisimulia siku ambayo ilimbidi atoke kwenye kivuko kinyume nyume kwasababu kilishindwa kusimama ipasavyo ikabidi kigeuke na hii ilikua nibaada ya kukaa majini kwa muda wa nusu saa wakati huo akiwa anahisi kwamba siku zake za kuishi zimekisha. Hii nisawa nakusema kwamba mwananchi ambaye anatumia Vivuko vya Kigamboni anaishi kwa matumaini kama mgonjwa wa ukimwi kwasababu japo ukweli ni kwamba kila anayesafiri anahatarisha maisha lakini kwao ni maradufu.

Vivuko vya Kigamboni vimechakaa na hii ina maana kwamba kila kitu ndani yake ni kibovu. Kwa mfano life jacket zimechakaa, milango ya kivuko inatakiwa ifungwe wakati kikiwa safarini lakini kinachofanyika ni “funika kombe mwanaharamu apite” ninasema hivi kwasababu wakati mwingine wanapitisha kamba nyembamba ya mkonge na wakati mwingine hakuna kizuizi chochote. Hii inamaanisha kama kivuko kikiyumbishwa na mawimbi kikainamia mbele au nyuma basi kama Guta au Gari likiteleza litazama bila kusita. Kwasababu kwa uelewa wangu mageti yaliyokuwepo sio mapambo. Nakama hayapo basi kunahatari inakuja.

Ni muda mrefu sasa tumekua tukiambiwa kwamba serikali inampango wa kubinafsisha vivuko vya Kigamboni kwa mmiliki binafsi ili aviboreshe. Wakati huohuo tunasia kuna mipango ya kujenga daraja, na hivi karibuni kulingana na habari zilizochapishwa kwenye gazeti moja la kila siku hapa nchini, serikali inampango wa kutafuta kivuko cha kukodi kwa muda wa miaka miwili. Hivyo basi Wizara ya Miundombinu imetangaza zabuni ikitafuta kampuni itakayoweza kukileta kivuko hicho nchini ambacho kitakua na uwezo wa kubeba uzito wa tani 170 hadi 250

Hapa kuna mambo kadhaa ambayo yanachanganya. Kwanza kunaubinafsishaji, pili kuna ujenzi wa daraja, tatu kuagizwa kivuko cha kukodi tena kwa muda wa miaka miwili. Sasa mimi najiuliza kama kuna mpango wa kujenga daraja yanini basi serikali iingie gharama ya kukodi kivuko? Kwanini hizo fedha zisitumike kujenga daraja? Lakini pia kwanini serikali itafute kivuko cha kukodi? Kwanini isinunue kivuko? Kwasababu takwimu zinaonyesha kwamba vivuko vya Kigamboni vinaiingizia serikali mamilioni ya shilingi. Vilevile vimefanya kazi kwa muda mrefu sana hivyo basi lazima vingekua vimeshazalisha fedha ya kununulia vingine.

Lazima tufahamu kwamba usafiri wa majini na anga ni hatari sana ukilinganisha na usafiri wa nchi kavu. Sasa hii inamaanisha kwamba inatakiwa umakini zaidi uongezwe kwenye vyombo vinavyosafiri angani na majini. Kwa mfano siku za karibuni kumeripotiwa ajali kadhaa za ndege hapa nchini. Lakini tofauti na gari, aghalabu ndege ikipata ajali inawaka moto hivyo basi kuwaokoa abiria huwa inakua ngumu. Itakumbukwa kwamba Marehemu Akukweti aliyekua Waziri kwenye serikali ya awamu ya nne ya Kikwete hatunayetena kutokana na majeraha ya kuungua aliyoyapata kwasababu ya ajali ya ndege.

Vile vile bado hatujasahau tukio la MV Bukoba. Sasa ndio maana tunahoji kwanini serikali inalifumbia macho la Kigamboni? Kwa sababu kama baya lolote litatokea kwa watumiaji wa vivuko vya Kigamboni wizara husika itabidi iwajibike. Wananchi hawatakubali kuambiwa eti ni bahati mbaya au ni mipango ya Mungu wakati hatua za tahadhari hazijachukuliwa.

Mimi huwa najiuliza hivi kama mwanafunzi anaenda shule kufanya mtihani wa taifa halafu ikatokea kwamba amekwama ndani ya maji masaa matatu, ni nani atafidia hasara hiyo? Na wakati mwingine tuchukue mfano wa mama mja mzito ambaye anawahishwa hospitali halafu akakwama ndani ya maji masaa matatu, akifa nani awajibike? Hili nalo tubaki kusema eti Mungu kapanga?

Inasikitisha kusikia kwamba wapo viongozi ambao waliapa kununu ndege ya rais hata kama wananchi watakula nyasi, wengine wakaenda kununu rada ya bei rahisi kwa bei ya kufuru. Hizo pasenti ambazo zinasemekana kwamba zilifanyiwa ubadhirifu pengine zingeweza kununua vivuko viwili au hata kujenga daraja kwa manufaa ya wananchi. Lakini serikali hiyo hiyo iliyofanya hayo ilishindwa hata kununua kivuko kimoja cha uhakika Kigamboni. Kwasababu ukiwaambia wananchi kwamba “fungeni mkanda tununue kivuko tuepushe maafa”, sidhani kwamba yupo atakaye lalamika.

Lakini siku zote falsafa ya Karl Max ya kutengeneza “the state of oppressed” (taifa la wanyonge) imekua ni falsafa ngumu sana. Karl Max anasema Serikali inayoongozwa na wanyonge ni muhimu kwasababu itabadilisha uchumi kutoka mikononi mwa mabepari na kuwapa wanyonge nafasi kubwa.

Wapo waliokua wanaiona serikali ya awamu ya tatu kama “the state of oppressed” lakini mambo hayajawa hivyo bado labda tuangalie siku za baadae. Kwa mfano bilioni 21 za Kikwete ni miongoni mwa mambo ambayo yalioonyesha umakini wa awamu ya nne katika kuwajali “the oppressed” lakini matatizo yameanza kuonekana, kwasababu wanaohusika na ugavi wa fedha hizo sio waadilifu. Tayari imeripotiwa kwamba wapo watu ambao wanakwenda kuomba mikopo hiyo nawanatakiwa watoe elfu kumi ili wapewe fomu za maombi.

Suala la Kigamboni ni miongoni mwa mambo ambayo yanaonyesha kwamba kunamapungufu makubwa katika utendaji kwenye wizara husika. Lakini falsafa ya “wakiambiwa hawaamini mpaka waone” ndio itakayo wazindua wahusika usingizini, lakini kwanini tufike huko? Kwa sababu sitaki kuamini kwamba serikali haina hela za kununua kivuko kipya kwasababu hata sisi hatusafiri bure. Sasa kama abiria wanalipa kwanini biashara haikui?

Hii ni aibu kwasababu kila siku tunaongelea masuala ya ujasiriamali, serikali inaeleza umuhimu wa kua na wajasiriamali kwa sababu wao ndio watapelekea kukuza uchumi. Lakini sasa inaonekana ndani ya Serikali kwenyewe ujasiriamali nikama nadharia ambayo haijaeleweka vizuri kwasababu miradi mingi ya serikali ukiwepo ule wa vivuko vya Kigamboni inaonyesha kwamba bado ujasiria mali upo katika maneno zaidi kuliko matendo.

Mjasiriamali anatakiwa awe na upeo mkubwa wa kubuni miradi, uwezo wa kumudu ushindani na kuweza kuziteka fikra za wateja ili awe na uhakika wa kukuza mtaji. Lakini ukweli kwamba biashara ya kuvusha abiria Kigamboni imeshikiliwa na serikali peke yao na hakuna kampuni jingine lolote linalofanya biashara hiyo, ndio maana serikali imeshindwa kua na ufanisi, kwasababu kinachotumika ni falsafa ya “ukitaka, usipotaka utapanda”. Ni sawasawa na wakati ule ilipokua CCM chama pekee cha siasa, kama ungeichukia CCM ungefanya nini? Kwani ukichagua kivuli kitakusaidia nini? Hivyo basi ilikua ni bora umchague mtu.

Mimi nadhani kama serikali imeshindwa kabisa ingeifanya biashara ya usafirishaji pale kivukoni ikawa huria. Yaani namaanisha iwe kama vile usafiri wa daladala, kila mwenye uwezo wa kuleta kivuko aruhusiwe kufanya biashara. Hapo nadhani serikali nayo ingechangamka kama vile uwepo wa vyama vya upinzani unavyotoa changamoto kwa CCM.

Lazima ifahamike kwamba nchi yetu ipo kwenye “mixed economy” nafikiri niuite (uchumi mseto) huu ni uchumi ambao nyanja za uchumi zinaendeshwa na wadau ambao wapo katika mafungu mawili (serikali na watu binafsi) hivyo basi nafikiri hakuna haja ya mdau mmoja kati ya wawili hawa kungangania kwamba yeye anayo haki ya kuendesha biashara mwenyewe.

Kwa mawazo yangu naiona Kigamboni kama sehemu nzuri sana ya kuishi, kwanza nikaribu sana na katikati ya jiji, pili ni pembezoni mwa bahari hivyo basi bila shaka kuna hewa nzuri inayosababishwa na upepo mwanana kutoka baharini. Lakini usafiri wa kusua sua umeifanya Kigamboni ionekane kama nguo nyeupe yenye doa kubwa jeusi.

Kutembea kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ni haki ya msingi kabisa ya mwanadamu. Lakini kwasababu huduma ya vivuko pale Kigamboni inaisha saa sita usiku inamaana kwamba mwananchi wa Kigamboni hana uhuru wa kutembea “freedom of movement” kwa sababu kama unafanya kazi zamu ya usiku na unatoka saa saba usiku, hapo unakua huna uhuru wakwendwa nyumbani labda ukalale kwenye nyumba za wageni.

Kabla sijaiweka chini kalamu yangu ningepenga kuikumbusha serikali ya awamu ya nne kwamba falsafa ya “Maisha bora kwa kila mtanzania” ingekua na maana zaidi kwa wananchi wa Dar es salaam kama wangejengewa daraja ili waepuke balaa ambalo huenda likawakumba wao ama ndugu zao na wageni kama vile watalii ambao hupenda kutembelea Kigamboni.

User Comments

http://www.kamsled.com it is a high-tech corporation specializing in high power LED lighting. Our products mainly include: led panel light,led tube,led light,led strip,led panel,led bulb light,led downlights,led strip light,led bulb,led bulbs,led lights

Post A Comment

This user has disabled anonymous commenting.